Bunge la Kaunti ya Kisii limejiongezea muda wa kujadili miswada kwa wiki mbili kabla ya kuenda likizoni.
Muda huo uliongezwa baada ya mwakilishi wa wadi ya Bombaba, Koina Onyancha, kuwasilisha mswada huo bungeni na kuungwa mkono na wawakilishi wadi wenzake.
Spika wa bunge la kaunti hiyo Okerosi Ondieki aliyasikiliza maoni ya wawakilishi hao walipokuwa wanajadili mswada huo siku ya Jumatano.
Spika huyo alipitisha mswada huo ili kuwawezesha kujadili mambo muhimu ambayo bado hayajashughulikiwa katika bunge hilo,
Kulingana na ripoti ya mswada huo, kuna miswada ambayo inastahili kujadiliwa kabla ya mwaka huu kukamilika.
Baadhi ya mambo muhimu yanayofaa kujadiliwa kabla ya mwaka kuisha ni uchunguzi wa miradi ambayo imefanywa na wawakilishi wa kaunti hiyo katika wadi zao, kujua jinsi miradi ya maendeleo imekuwa ikifanyika katika wadi, masuala ya uajiri katika serikali ya kaunti hiyo na kupitisha miswada ambayo imejadiliwa na haijapitishwa kati ya mambo mengine mengi.
Wawakilishi hao walipaswa kuenda likizoni kuanzia Disemba 3, 2015 hadi Januari 2, 2015 lakini sasa wataenda likizo hiyo kuanzia tarehe 17 Disemba 17, hadi tarehe Januari 12.
“Vikao vya wawakilishi wa bunge hili vitaendelea hadi tarehe Disemba 17 ili tujadili masuala muhimu kabla ya mwaka kukamilika,” alisema Ondieki.