Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la Kaunti ya Kisii limepitisha mswada wa kuanzisha hazina ya watu wanaoishi na ulemavu pamoja na ya ile ya akina mama.

Mswada huo ulipitishwa siku ya Jumatano baada ya idadi kubwa ya wawakilishi wadi kuunga mkono.

Mswada huo ulifikishwa bungeni na kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo Protus Moindi, ambaye alisema kuwa hazina hiyo ikianzishwa itakuwa inatoa usaidizi kwa watu wanaoishi na ulemavu na akina mama ambao hufanya biashara ili kujiendeleza.

“Tumeona walemavu wengi na akina mama wakiteseka kwa kukosa njia za kujitafutia riziki ya kila siku, pamoja na kukosa pesa za serikali ya kaunti zitakazo wasaidia kuanzisha biashara na kujiendeleza kimaisha kupitia biashara hizo,” alisema Moindi.

Aliongeza, “Hazina hii itatoa usaidizi kwao kwani kwa sasa walemavu hupata usaidizi kutoka kwa serikali ya kitaifa. Kuna haja ya serikali ya kaunti kutoa usaidizi wa aina hiyo ili kuwawezesha kujiendeleza.”

Mswada huo ulipitishwa rasmi bila kupigwa na spika wa bunge hilo Okerosi Ondieko baada ya kupokelewa kwa moyo mmoja.

Sasa kile ambacho kimesalia ni mswada huo kutiwa sahihi na Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ili kuwa sheria.

Mwakilishi wa watu wanaosishi na ulemavu katika kaunti hiyo Felstas Metobo alimwomba Gavana Ongwae kuharakisha kuutia sahihi mswada huo ili kuwa sheria.