Bunge la Kaunti ya Nyamira limepitisha mswada wa kutengea maeneo wadi ishirini ya kaunti hiyo shillingi millioni 368, pesa zitakazo saidia kustawisha maendeleo mashinani.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiwasilisha mswada huo bungeni siku ya Alhamisi, mwakilishi wa wadi ya Gesima Ken Atuti alisema pesa za ustawishaji wa maeneo wadi zitasaidia kupanua barabara mashinani na hata pia kuwawezesha mayatima kufadhiliwa kupata elimu.

"Mswada huu ambao tumeupitisha ili kutengea maeneo wadi pesa za kustawisha Maendeleo ni mswada muhimu. Pesa hizo sio za kutusaidia sisi wawakilishi wadi bali ni za kusaidia kupanua barabara mashinani na hata pia kuwasaidia watoto werevu hasa mayatima kufadhiliwa kupata elimu," alisema Atuti.

Atuti aidha aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuwa macho ili kuhakikisha pesa hizo zinawafaidi wakazi pindi tu zitakapo idhinishwa na gavana wa kaunti hiyo.

“Ni himizo langu kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanakuwa macho pindi tu pesa hizi zitakapo tolewa ili kuhakikisha kuwa zinatumika kutekeleza miradi muhimu na wala sio kwa kuwafaidi watu binafsi,” aliongezea Atuti.