Viongozi wakuu serikalini wamekosolewa kwa kushindwa kuangazia swala la usawa wa kijinsia wa thuluthi mbili nchini.
Kulingana na Mkurungezi mkuu wa Shirika la kijamii la Coast Women in Development, Betty Sharon, tangu wanaharakati mbalimbali na mashirika ya kijamii kujitokeza kupigania swala hilo, bunge na serikali haijaonyesha ari ya kubadilisha uongozi wa taifa hili.
Akiongea katika mkutano wa wanawake mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Bi Sharon alisema bunge linafaa kuurudisha mswada huo bungeni na kuujadili vyema ili kuona kwamba swala la jinsia na haki za wanawake nchini zinaangaziwa.
Alisema iwapo swala hilo litasaulika basi haki za wananwake nchini hususan swala la thuluthi mbili la usawa wa jinsia katika uongozi litakosa kuangaziwa na bunge la kitaifa litakuwa limekiuka Katiba ya nchi.
“Tumeona wazi kwamba bunge la kitafa na serikali kuu imekosa kuangazia vyema swala la usawa wa kijinsia wa thuluthi mbili na hatua hiyo basi imeonyesha wazi kwamba wanawake wanazidi kukandamizwa katika maswala ya uongozi nchini," alisema Bi Sharon.
Wakati huo huo, Bi Sharon aliwashiniza wanawake kuungana na kulishinikiza bunge la kitaifa, Mkuu wa Sheria Profesa Githu Muigai na viongozi wa kisiasa kuangazia swala hilo ili kumpa fursa mwanamke kulitumikia taifa.
Mwanaharakati huyo wa kijamii aliahidi kuzuru sehemu mbalimbali za eneo la Pwani kuwahamisisha wananwake jinsi ya kutetea haki zao za kimsingi pamoja na kupigania swala la usawa wa kijinsia katika uongozi wa thuluthi mbili.