Kufuatia baadhi ya walimu wakuu wa shule za umma kudinda kupunguza viwango vya karo vinavyotozwa wazazi kwa minajili ya elimu ya wanao, baadhi ya wazazi kutoka maeneo mengi Kaunti ya Nyamira kupitia kwa muungano wa chama cha wazazi eneo hilo wanapanga kufanya maandamano kulalamikia hali hiyo.
Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa chama cha wazazi tawi la Nyamira Vincent Mbura alisema kuwa iwapo shule za umma zitadinda kupunguza kiwango cha karo, wazazi watalazimika kufanya maandamano hadi kwa afisi za wizara ya elimu kaunti hiyo.
"Serikali ilikuwa imetoa kiwango rasmi cha karo kinachostahili kulipwa katika shule mbalimbali za umma, lakini baadhi ya shule zingali zimekiuka agizo hilo, na iwapo walimu wakuu wa shule husika hawatapunguza viwango hivyo vya karo, basi tutalazimika kuandamana hadi kwenye afisi za wizara ya elimu Nyamira," alionya Mbura.
Mbura aidha aliongeza kusema kuwa hatua ya shule za umma kuongeza karo ni njia mojawapo ya kuwabebesha mizigo zaidi wazazi ikizingatiwa kuwa hali ya uchumi inaendelea kudorora nchini, huku akihoji kuwa kamwe hilo halitakubalika.
"Hatuwezi kamwe kuketi tukiangalia shule zikiongeza karo kiholela kwa kuwa hii ni njia mojawapo ya kuwabebesha wazazi mizigo zaidi ikizingatiwa kuwa hali ya uchumi wa taifa hili inaendelea kudorora," alihoji Mbura.