Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha ODM kimeanzisha mchakato wa kuwasajili wanachama wake kwenye maeneo mbalimbali ya kibiashara katika kaunti ya Nyamira, huku wakitarajia kuwasajili vijana wengi zaidi kwenye zoezi hilo linalotarajiwa kutamatika baada ya siku ishirini. 

Akiongea wakati wa kuanzishwa zoezi hilo la usajili nje ya afisi za chama cha ODM mjini Nyamira, afisa wa uhusiano mwema wa chama hicho Stella Nyaundi alisema kuwa zoezi hilo linatarajia kuwasajili wanachama sawia kutoka wadi zote ishirini kaunti ya Nyamira ili kuhakikisha kuwa kutakuwa na usawa kwenye uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu. 

"Tuko macho, kuhakikisha kuwa kila eneo limepata madeligeti na wanachama sawia watakaoruhusiwa kupiga kura, na hii ni kwa sababu tunataka kuepuka visa ambapo baadhi ya wagombezi nyadhifa mbalimbali hukosa imani ya uchaguzi wa huru na haki," alisema Nyaundi. 

Afisa huyo aidha aliwaonya vikali wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali kuingilia kazi ya maafisa wanaotekeleza shughuli hiyo ya usajili ili kuhakikisha kuwa wanapendelewa, huku akisema kuwa kamwe hilo halitoruhusiwa. 

"Wale wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali wanaodhani kuwa watawashurutisha maafisa wa usajili kusajili wanachama zaidi kuliko idadi iliyowekwa, kamwe hilo halitoruhusiwa kwa kuwa sisi tunatarajia vijana wengi kujisajili kwenye zoezi hili," alionya Nyaundi. 

Maeneo ambayo zoezi hilo linatarajiwa kufanyika ni Keroka, Nyansiongo, Kebirigo, Manga, Nyamusi na Nyaramba.