Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, amesema ili kudhibiti ufisadi humu nchini, ni lazima viongozi wote wanaojihusisha na uhalifu huo wachukuliwe hatua za kisheria.

Sheikh Khalifa alisema kuwa ufisadi umekithiri mno humu nchini huku viongozi wakuu serikalini wakihusishwa na kashfa hizo.

Akizungumza na mwanahabari huyu afisini mwake mjini Mombasa siku ya Ijumma, kiongozi huyo wa kidini alisema kuwa hali hiyo ni ya kusikitisha mno, na kusisitiza kuwa ni lazima vita dhidi ya ufisadi vikabiliwe kikamilifu ili kulinda mali ya umma.

Aidha, aliikosoa Tume ya EACC kwa kuzembea katika kuyatelekeza majukumu yake.

Sheikh khalifa ameitaka tume hiyo kuwahakikishia Wakenya kuwa ina uwezo wa kuwakabili viongozi na maafisa wote wa umma wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali ya umma.

“Tunashindwa kuelewa jinsi Tume ya EACC inavyotekeleza wajibu wake, kwa sababu kashfa za ufisadi zimezidi na zinaendelea kuharibu uchumi wa nchi kwani hata viongozi na maafisa walio serikali ni wafisadi. Hili ni jambo la kusikitisha mno,” alisema Sheikh Khalifa.

Lalama za mhubiri huyo wa dini ya Kiislamu zinajiri huku sakata za ufisadi za Shirika la huduma kwa vijana NYS na ile inayomuandama Jaji wa mahakama ya upeo nchini Philip Tunoi zikichukua mkondo mpya.