Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katibu wa Baraza la Maimam nchini CIPK Sheikh Mohammed Khalifa amewahimiza viongozi wa kidini, viongozi wa mitaa pamoja na wazazi kushirikiana na mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa na idara ya usalama kwa jumla, kukabiliana na ukosefu wa usalama ambao umekithiri katika Kaunti ya Mombasa.

Akizungumza na waandishi wa habari afisini mwake siku ya Jumanne, Khalifa, aliwataka wazazi kutoa habari muhimu kwa idara ya usalama ikiwemo kuwataja vijana wanaodaiwa kuwahangaisha wananchi ili kuwawezesha maafisa wa polisi kuwatia nguvuni.

Kiongozi huyo wa kidini aliwasuta wazazi kwa kile alichokitaja kama kusalia kimya licha ya kuwatambua vijana wanaoendeleza uhuni, huku wengine wakiwaficha badala ya kutoa ripoti kwa idara ya usalama.

Aidha, Khalifa alikilaani vikali kitendo ambacho mama mmoja anadaiwa kuvulia nguo na vijana wa makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao katika eneo la Sokomjinga siku ya Jumapili.

Visa vya wananchi kuhangaishwa na makundi ya uhalifu mjini Mombasa vimeripotiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni, huku makundi ya vijana ya Wakali Kwanza na Wakali Wao yakidaiwa kuyatekeleza maovu hayo hata nyakati za mchana.