Baraza la Maimam na Wahubiri nchini CIPK limeunga mkono hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza vita dhidi ya maafisa wa umma wanaoshiriki ufisadi.
Kwenye makao na wanahabari katika afisi za baraza hilo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Katibu mtendaji katika baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa alimtaka Rais Kenyatta kutumia mamlaka yake kikatiba kuwakabili maafisa wafisadi kwani taifa hili limerudi nyuma kimaendeleo kufuatia ufujaji wa mali ya umma.
Sheikh Khalifa alisema kwamba iwapo rais atachukua jukumu la kupigana kikamilifu na wafisadi nchini, basi taifa hili litaimarika kiuchumi.
Alimtaka rais kuzishinikiza idara fisadi kurudisha mara moja fedha za umma zilizofuja katika afisi za serikali ili mwananchi kufaidika.
Wakati huo huo amepinga vikali hatua ya kuongeza ushuru kwa wananchi kama njia moja wapo ya kukabiliana na ufisadi, na akaitaka idara ya mahakama na afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma nchini kutii agizo la rais na kuanza jukumu la kupambana na wafisadi.
"Tunamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kwa kujitokeza waziwazi na kutangaza vita vikali dhidi ya maafisa wa umma wafisadi. Tunamsihi atumie mamlaka yake kama raisi kikatiba kuwakabili maafisa wafisadi ili kulinda mali ya umma na kuliokoa taifa hili kutoka janga la ufisadi,” alisema Sheikh Khalifa.
Mapendekezo ya Baraza hilo la CIPK yamejiri siku moja tu baada ya Rais Uhuru kenyatta kulihutubia taifa na kutangzaa ufisadi kuwa janga la kitaifa.