Mwenyekiti wa maktaba nchini Samwel Nyangeso amehimiza muungano wa upinzani Cord, kushirikiana na serikali ili kuleta maendeleo kwa Wakenya.
Kulingana na mwenyekiti huyo, muungano wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga, hauna budi ila kushirikiana na serikali ikiwa muungano huo unahitaji kuhakikishia Wakenya maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumapili mjini Kisii, Nyangeso aliomba upinzani kuweka siasa kando na kushirikaiana na serikali ya Uhuru Kenyatta kunufaisha Wakenya kimaendeleo badala ya kufanya siasa zizizo na msingi wowote.
“Naomba Raila na muungano wake kushirikiana na serikali ili kuleta maendeleo kwa Wakenya. Wakenya wanahitaji maendeleo ili tuweze tujenge nchi yetu. Tuasi mambo ya siasa kwa sasa kwa vile wakati wa siasa bado haujafika,” alisema Nyangeso.
Hata hivyo, Nyangeso alikosoa muungano wa Cord kwa kuendelea kutumia madai ya ufisadi serikalini kuikosoa serikali kila siku na kusema hilo halitawanufaisha Wakenya kwani wanachohitaji wananchi ni maendeleo.
“Haya mambo ya kuendelea na siasa hayawezi kutusaidia vyovyote humu nchini. Sisi sote tunastahili kuungana na kushirikiana na serikali ili kuleta maendeleo,” alisisitiza Nyangeso.