Share news tips with us here at Hivisasa

Visa vya dhulma za kimapenzi na kijinsia katika kaunti ya Nakuru viomeongezeka kwa kiwango kikubwa, huku wito ukitolewa kwa polisi kuchunguza wahusika na kuwashtaki.

Wiki mbili tu baada ya msichana wa mika sita kubakwa katika eneo hilo, mwanamme mwenye umri wa makamo ametiwa mbaroni katika eneo la Marigo B Solai kaunti ya Nakuru kwa madai ya kumbaka nyanya mwenye umri wa miaka 80 mnamo Jumatatu.

Mshukiwa huyo alifumaniwa nyumbani mwa nyanya huyo, baada ya kuchimba shimo na kuingia kwenye nyumba ya nyanya huyo.

Mkaazi mmoja, Elizabeth Ongiri alisema walimkamata kijana huyo baada ya kufungua mlango kwa hiari.

“Nilipigiwa simu na jirani aliyeskia nyanya huyo akipiga mayowe, na nilipofika kwa hiyo nyumba pamoja na majirani, nikamulika kupitia shimo hilo na nikamfahamu mshukiwa. Tulipotaka kuvunja mlango akasema kwa hiari atafungua. Alikuwa amekalia kitanda cha nyanya huyo,” alisema.

“ Anafanya kazi ya kuchimba mawe kwenye karakarana za hapa na sio mara ya kwanza ya kijana huyo kuhusishwa na maswala ya ubakaji," mkaazi mwingine John Gacheru alisema.

Wanakijiji walimpeleka nyanya huyo katika hospitali ya wilaya ya Bahati iliyo Maili Kumi, ambapo madaktari walidhibitisha kubakwa kwake.

Mshukiwa alizuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Solai, na anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo, Jumatano.

“Kijana huyu ameleta laana kwa kijiji chetu. Tungetaka mahakama imfunge hata kama ni maisha ili aondolee jamii aibu,” alisema mkaazi mwingine, Margaret Wanjiru.