Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi kutoka katika maeneo mbali mbali eneo la Pwani wametakiwa kupigana vita dhidi ya matumizi na usambasaji wa dawa za kulevya, na kuhakikisha kuwa wale wanaohusika wanatiwa mbaroni na kushtakiwa.

Akiongea siku ya jana Jumamosi katika shule moja kwenye hafla ya mchango, kiongozi wa walio wengi katika bunge la taifa Adan Duale alipongeza juhudi za idara za usalama na mashirika ya kijamii kwa juhudi zao za kuhakikisha kuwa jinamizi hilo la mihadarti linaangamizwa kabisa.

Aidha aliwataka wazazi pamoja na mashirika mengine katika kaunti husika kushirikiana na serikali ya taifa na ile ya Kaunti ili kupunguza kuenea kwa dawa za kulevya na matumizi yake.

Kiongozi huyo wa Jubilee alifafanua umuhimu wa kila kiongozi kuwa tayari kulikabili zogo hilo, ambalo alitaja kuwa changamoto kuu kwa kutoendelea miongoni mwa vijana hali ambayo imechangia pia kurudi nyuma kwa Kaunti hizo za eneo zima la Pwani.

“Kama mmeweka juhudi za kuwatambua wanaotumia dawa za kulevya katika kaunti za hapa, fanya bidii ya kuwatambua wale wahusika wakuu katika kuuza na kusambaza mihadarati kwa vijana na kina mama katika kaunti za eneo la Pwani kwa jumla,” alisema Duale.