Kufuatia shambulizi la hivi majuzi la wanamgambo wa Alshabab katika eneo la El Adde nchini Somalia na kupelekea kuuwawa kwa wanajeshi wa Kenya KDF, sasa viongozi wa serikali wanapendekeza kuongezwa wanajeshi wengine zaidi ili kuimarisha usalama.
Akiwahutubia wakaazi wa eneo la Pwani siku ya Jumanne, Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale amesema kuwa serikali haipaswi kuingiwa na uoga kufuatia shambulizi hilo na badala yake inafaa kukabiliana vikali na wanamgambo hao ili usalama kuimarishwa zaidi.
Duale amehoji kuwa kuimarika kwa taifa la Kenya kiusalama kunatokana na kuimarika kwa mataifa jirani kiusalama na hali hiyo itainua uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa.
“Tunapendekeza serikali kuhakikisha kuwa imeongeza wanajeshi wengine Somalia kukabiliana na hawa jamaa na kuimarisha usalama katika mipaka yetu na hatua hiyo itasaidia kuinua uchumi wa nchi,” alisema Aduale.
Naye waziri wa usalama wa ndani, Meja Mstaafu Joseph Nkaiserry, amesema kuwa usalama umeimarishwa kote nchini, na akaahidi kuwa serikali itatumia kila mbinu kuwaangamia wananmgambo wa Alshabab ambao wamekuwa tishio kwa wananchi.