Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa Mombasa wanaitaka tume ya EACC kuharakisha katika kushughulikia sakata ya ufisadi ya ‘Chicken gate’.

Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Ijumaa, wakiongozwa na Saudina Hamisi, wakazi wa Kongowea walisema kuwa tume hiyo inajikokota katika kuweka wazi waliohusika katika sakata hiyo.

Aidha, wametaka hatua za kisheria kuchukuliwa kwa watakaopatikana na hatia ya kuhusika katika sakata hiyo ya ‘Chicken gate’.

Kauli hii inajiri baada ya tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, kudokeza kuwa wamepata stakabadhi za ushahidi kutota nchini Uingereza kufuatia usaidizi wa kisheria katika sakata ya ufisadi ya ‘Chicken gate’.

Mwenyekiti wa tume hiyo Philip Kinisu, alisema kuwa faili ya stakabadhi hizo ziliwasilishwa humu nchini mwezi uliopita na uchunguzi umepiga hatua huku tume hiyo ikitarajiwa kutoa mapendekezo yake katika wiki mbili au tatu zijazo.

Taarifa hiyo mpya itasaidia kuthibitisha endapo maafisa wa iliyokuwa tume ya muda ya uchaguzi na mipaka nchini IIEC walihusika kikamilifu katika sakata hiyo ya ufisadi.

Nchini Uingereza, maafisa wawili wa kampuni ya Smith & Ouzman walipatikana na hatia ya kuwahonga maafisa wa tume ya uchaguzi nchini na wakahukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani kila mmoja.

Mwenyekiti wa tume ya IEBC Issack Hassan, aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo James Oswago, Davis Chirchir, miongoni mwa maafisa wengine walitajwa katika sakata hiyo.