Halmashauri ya Bandari nchini KPA imesema kuwa eneo la 21 la kuegesha meli linatarajiwa kuanza shughuli za upakuzi na usafirishaji wa mizigo, kwani meli za mizigo zinatarajiwa kuwasili na kutia nanga katika bandari hiyo.
Afisa wa Mawasiliano katika Halmashauri ya Bandari ya Mombasa KPA, Hajj Masemo alisema kuwa eneo hilo limekamilika na linaweza kuanza shughuli za upakuaji wa migizo.
Hatahivyo, alisema kuwa vifaa zaidi vinatarajiwa kuwasili katika bandari hiyo ili kukamilisha sehemu zingine zilizosalia.
Masemo alisema kuwa kwa ushirikiano wa halmashauri ya KPA na serikali kuu kupitia wizara ya uchukuzi na muundo msingi, shughuli hiyo imefanikiwa na huenda uchumi wa taifa hili ukaimarika zaidi kwa kuwa shughuli za kibiashara zinatarajiwa kuimarika mara dufu.
Akizungumza na mwanahabari mjini Mombasa siku ya Jumapili, Masomo alisema kuwa kwa sasa anasubiri Rais Uhuru Kenyatta kufika katika eneo hilo kwenye Bandari ya Mombasa kufanya ukaguzi rasmi.
“Rais Uhuru Kenyatta bado hajafika katika eneo hili kukagua kukamilika kwa shughuli ya ujenzi. Hata hivyo, meli za mizigo zinaweza anza kutia nanga katika sehemu hiyo kwani kila kitu kimekamilika. Tunatarajia meli zile kubwa zaidi zenye urefu wa mita 250 hadi mita 300,” alisema Masemo.
Bandari ya Mombasa sasa ni kati ya bandari tano bora barani afrika zilizo na uwezo wa kuegesha meli kubwa zaidi zenye urefu wa mita 300 na zaidi, kutokana na upana na urefu wa bandari hiyo.