Share news tips with us here at Hivisasa

Huku ziara ya Rais Uhuru Kenyatta katika ukanda wa Pwani ikitarajiwa kutamatika mwishoni mwa wiki hii, msemaji wa Ikulu Manoa Esipisu tayari ametao taarifa kuwa rais anapanga kurejea tena kukamilisha aahadi alizotoa wakati wa kampeni.

Katika kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Esipisu, alisema kuwa rais ameratibu kuzuru Pwani tena siku zijazo ili kuikamilisha miradi ambayo hakuweza kuitekeleza.

“Rais Kenyatta atarudi kuzitembelea kaunti za Taita Taveta, Tana River na Kwale katika ziara yake ya pili katika ukanda wa Pwani. Wanaopiga siasa wacha waongee lakini rais atazidi kuutekeleza wajibu wake,” alisema Esipisu.

Esipisu alisisitiza kuwa ziara ya rais katika eneo hilo haikuwa ya kisiasa ila ya kutekeleza agenda na ahadi ambazo mrengo wa Jubilee ulitoa wakati wa uchaguzi uliopita.

Aidha, aliongeza kuwa serikali imeweka mikakati thabiti ili kuhakikisha kuwa usalama katika eneo la Pwani na sehemu zingine nchini unaimarishwa.

Esipisu vilevile alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo Rais anapania kuyatekeleza Pwani ni pamoja na ukarabati wa shule ya msingi ya Jomo Kenyatta iliyooko Msambweni, Kaunti ya Kwale.

Aliongeza kuwa katika siku za hivi karibuni rais atazuru maeneo mbalimbali nchini katika hatua ya kuhakikisha kuwa kila eneo linafaidi kimaendeleo.

“Rais anapanga kufanya kazi akiwa mashinani, kwa hivyo mumtarajie mlangoni mwako,” alisema Esipisu.