Share news tips with us here at Hivisasa

Familia moja kutoka eneo la Ngomongo, Kaunti ya Nakuru, imedai kukataliwa na jamii kufuatia kuvamiwa na wadudu aina ya funza.

Familia hiyo ya Bw James Macharia imedai kushurutishwa kuhama mahala pao pa maakazi na chifu wa eneo hilo kwa misingi kuwa wanatoa taswira mbaya ya eneo hilo.

Familia hiyo ilidai kuwa chifu huyo alisema kuwa eneo la Ngomongo kamwe halitakuwa na historia ya kuvamiwa na wadudu hao.

Familia hiyo iliyo na watoto sita aidha inaripotiwa kukumbwa na masaibu mengi ikiwemo kushindwa kulipa kodi ya nyumba, huku ripoti zikiarifu kuwa Bi Macharia ambaye ni mhadhiriwa mkuu wa wadudu hao, hulazimika kufungiwa kwa nyumba kufuatia janga hilo.

Inasemekana kuwa watoto wa familia hiyo hukosa kwenda shuleni kutokana na kuvamiwa na funza hao.

Hata hivyo, kulingana na Mbugua Njau, ambaye ni mwenyekiti wa wahudumu wa afya katika jamii, alisema kuwa familia hiyo iliyohama kutoka eneo la Solai, Kaunti ndogo ya Subukia miezi miwili iliyopita, inaishi katika hali ya kutamausha.

"Kama maafisa wa afya tumejaribu kutoa suluhu katika janga hilo, japo hali hiyo bado haijathibitika maanake hatuna dawa kamili ya funza hao," alisema Mbugua.

Naibu kamishna wa eneo la Dundori Stephen Makwi, alikana madai hayo akisema kuwa uchunguzi ulibaini kuwa taarifa hiyo ni uvumi tu.

Makwi alisema kuwa tayari angekuwa amechukua hatua ya kinidhamu dhidi ya chifu huyo iwapo taarifa hiyo ingekuwa na ukweli wowote.

"Nilipomuita chifu huyo, aliweza kueleza kuwa hakuwa ametishia kufurusha familia hiyo. Nafikiri ilikuwa ni uvumi tu. Kumekuwa na funza katika eneo hilo lakini tunasaidiana na naibu chifu kumaliza wadudu hao," alisema Makwi.