Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nyamira amekosolewa kwa kuchelewa kuwasilisha ripoti ya uchungunzi iliyofanywa na kamati iliyochaguliwa kuchunguza miradi ya maendeleo yanayofanywa na idara za kaunti hiyo.

Kamati hiyo ilichaguliwa mapema mwaka huu na Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ili kuchunguza miradi ya maendeleo huku ripoti ya kamati hiyo ikisubiriwa kuwasilishwa kwa wabunge wa kaunti hiyo kwa muda mrefu sasa.

Ripoti hiyo inapaswa kuwasilishwa katika bunge hilo na Gavana Nyagarama lakini hadi sasa haijawasilishwa, jambo ambalo limesababisha wawakilishi wadi kumkosoa gavana kwa madai ya kurudisha maendeleo nyuma.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika bunge la Kaunti ya Nyamira kiongozi wa walio wachache katika bunge hilo Jackson Mogusu, alishangazwa ni kwa nini ripoti hiyo haijafika katika bunge hilo tangu kamati ichaguliwe kufanya uchunguzi huo.

Kiongozi huyo aliungwa mkono na wawakilishi wa bunge hilo na kumwomba Gavana Nyagarama kuwasilisha ripoti hiyo ili waweze kubaini miradi ya maendeleo inavyoendelea.

“Tunahitaji ripoti hiyo tuone jinsi miradi ya maendeleo ilifanywa na jinsi itafanywa kwa kaunti yetu. Hakuna haja ya gavana kukawia kuwasilisha ripoti hiyo,” alisema Jackson Mogusu.

Spika wa bunge la kaunti hiyo Joash Nyamoko alisema atajaribu kila awezalo kuhakikisha ripoti hiyo imewasilishwa na gavana juma lijalo ili kuona yale kamati hiyo iliyoyachunguza.