Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewaonya maafisa wa serikali ya kaunti wanaotumia magari ya serikali dhidi yamatumizi mabaya ya mafuta.
Akizungumza afisini mwake siku ya Jumanne, Gavana Nyagarama aliwaonya maafisa hao dhidi ya kuishi mbali na mji wa Nyamira.
Gavana huyo alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo imekuwa ikipoteza mamillioni ya pesa za umma kupitia kwa matumizi ya mafuta yanayoweza kuthibitiwa.
"Kwa mara nyingi nimekuwa nikiwaambia kuwa yafaa muishi karibu na mji ili kuthibiti matumizi ya mafuta, lakini bado hamjatimiza hilo. Kamwe hilo halitaruhusiwa na iwapo magari ya kaunti lazima yaende nje, yataenda tu kwa minajili ya shughuli rasmi," alisema Nyagarama.
Nyagarama alisema kuwa maafisa watakaoruhusiwa kuishi mbali na mji wa Nyamira watalazimika kutumia magari yao ya kibinafsi.
Alisema kuwa watakao kiuka agizo hilo watachukuliwa hatua kali.
"Tunataka kupunguza matumizi ya pesa za umma na ndio maana tunataka maafisa wetu waishi karibu na mji wa Nyamira. Hatuwalazimishi kufanya hivyo ila afisa yeyote anayetaka kuishi mbali na Nyamira sharti atumie gari lake la kibinafsi. Iwapo yeyote atakiuka agizo hilo, awe tayari kuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Nyagarama.