Wakazi wa mtaa wa Majaoni, Kisauni siku ya Alhamisi walipata fursa ya kusherehekea baada ya kuona matunda ya mradi walioanzisha miaka kadhaa iliyopita.
Wakazi hao walijumuika pamoja na waalimu na wanafunzi katika shule ya Valerye McMillan eneo hilo wakati wa sherehe za kuwatuza wanafunzi wa kwanza kufaulu kukamilisha mtihani wa kitaifa wa KCPE.
Gavana wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho pamoja na viongozi wengine waliungana na waalimu pamoja na wanafunzi katika sherehe hizo zilizotajwa kama mafanikio makubwa ya mradi huo.
Akiongea baada ya sherehe hizo,Gavana Joho aliwapongeza wanafunzi waliofanikiwa kukamilisha masomo ya darasa la nane, akisema kwamba ni ishara kwamba juhudi zao za kuanzisha shule hiyo zimeanza kuonekana.
“Tulianza na mradi wa kuwapa watoto chakula, kisha wazo la kuanzisha shule likatokea na hapo ndipo shule hii ilizaliwa. Ningependa kuwashukuru wote waliochangia katika mafanikio haya,” alisema Joho.
Wanafunzi hao wapatao 34 ndio wa kwanza shuleni humo kufanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka jana, miaka kadhaa baada ya shule hiyo kuanzishwa eneo hilo.
Shule ya Valerye ilianzishwa miaka ya nyuma kwa ushirikiano wa Gavana wa Hassan Joho aliyekuwa wakati huo mbunge wa Kisauni, pamoja na mchango kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo.
Wakati huo huo pia gavana ameahidi kuendelea kushirikiana na usimamizi wa shule katika kusaidia kuimarisha elimu kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo na Mombasa kwa ujumla.