Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewahimiza wapinzani wa uongozi wake kuungana naye katika kustawisha maendeleo ya kaunti hiyo.
Akiongea kwenye hafla ya kuchangisha pesa za kujenga hospitali ndogo ya Borabu siku ya Ijumaa, Nyagarama alisema kuwa badala ya wapinzani wake kushinda wakiikosoa serikali yake, inafaa waungane na kutekeleza miradi inayoweza kuimarisha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo.
"Haifai kila mara iwe sisi wanasiasa ni kupiga siasa za kulumbana, inafaa tujiungie pamoja ili tufanye miradi inayoweza kustawisha maisha ya wananchi kwa njia moja ama nyingine," alisema Nyagarama.
Gavana huyo aidha ameongeza kwa kusema kuwa kwa sasa hospitali kuu ya Nyamira ina mashine ya kuosha damu ya walio na shida ya figo, na aliwahimiza wale ambao wamekuwa wakisafiri kwenda sehemu zingine kupokea huduma hizo muhimu waitembelee hospitali kuu ya Nyamira ili kutibiwa.
"Tayari tusha ezeka mashine ya CT SCAN na nyingine ya kuosha damu kwenye hospitali kuu ya Nyamira, na ninawahimiza wananchi ambao wamekuwa wakienda kaunti zingine ili kupokea huduma hizo kutembelea hospitali kuu ya Nyamira ili wapate matibabu," alisema Nyagarama.
Akizungumzia swala la kusaidia kujenga hospitali ya Kijauri Nyagarama alisema kuwa serikali yake itatoa shillingi millioni kumi ili kuiwezesha hospitali hiyo kujenga wadi za wagonjwa, na maabara.
"Serikali yangu itatoa shillingi millioni kumi ili kuiwezesha hospitali hii kujenga wadi za wagonjwa pamoja na maabara ya kisasa," aliongeza.
Hafla hiyo ilifanikisha kuchangisha shillingi 950,000 pekee.