Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Chache Kusini, Richard Onyonka, amemuomba Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae kutowaruhusu wakuu wa idara wanaohusishwa na ufisadi kusalia afisini.
Onyonka alisema gavana anastahili kuweka kando masuala ya kisiasa na kuwapiga kalamu wakuu wa idara ambao watahusishwa na masuala ya ufisadi na utepetevu wa kikazi.
Akizungumza mjini Kisii siku ya Ijumaa, Onyonka alimwomba Gavana Ongwae kuwafuta kazi wakuu wa idara ambao hawawajibiki kikazi kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo.
“Gavana wetu anapaswa kuwapiga kalamu wakuu wa idara wanaohusishwa na ufisadi na wanao zembea kazini kama njia moja ya kuhakikisha kuwa wakazi wa Kisii wanapata huduma bora,” alisema Onyonka.
Kulingana na Onyonka, wakuu wa idara katika kaunti walichaguliwa kutumikia wananchi lakini iwapo hawatafanya kazi kwa kiwango kinachostahili, wanapaswa kupigwa kalamu.
Wakati huo huo, Onyonka aliwahimza wakuu wa idara kufanya kazi ili kuepuka kusimamishwa kazi na kuwataka kuenda mashinani kufanya kazi kikamilifu.