Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la Kaunti ya Nyamira limemtaka Gavana John Nyagarama kuweka wazi ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoteuliwa kuchunguza madai ya ufisadi yaliyokuwa yakiwakabili wakuu wa idara wanne na makatibu wawili.

Wakijadili hoja hiyo bungeni siku ya Jumatano, wawakilishi wadi walimtaka Gavana Nyagarama kuelezea sababu za kutowekwa wazi kwa ripoti hiyo, ili kuwawezesha wananchi kufahamu ukweli.

Spika wa Bunge hilo Joash Nyamoko, alimwagiza karani wa bunge la kaunti hiyo Daniel Orina kumwandikia barua Katibu wa Uajiri wa kaunti hiyo Erick Aori kuagiza kuwasilishwa kwa ripoti hiyo.

"Kwa kuwa katibu wa uajiri katika kaunti hii amekataa kuwasilisha ripoti ya kamati teule iliyoteuliwa kuwachunguza wakuu wa idara wanne na makatibu waliokuwa wamehusishwa na ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka, sasa ni jukumu langu kumwagiza karani wa bunge kumwandikia katibu wa uajiri barua ya kumtaka kuwasilisha ripoti hiyo bungeni,” alisema Nyamoko.

Nyamoko vilevile ameiagiza Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mwenyekiti wa Kamati Spesheli James Sabwengi kuchunguza pesa zilizotumika na maafisa wakuu wa serikali hiyo katika ziara ya kuzuru mataifa ya Italia na Marekani.

"Sharti kamati ya uwekezaji kwa ushirikiano na kamati spesheli ichunguze kiwango cha fedha zilizotumika na maafisa wakuu wa serikali ya kaunti hii kuzuru mataifa ya Italia na Marekani,” alisema Nyamoko.

Aidha, ametaka matokeo ya uchunguzi huo kuwasilishwa bungeni chini ya wiki mbili zijazo.