Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amewashauri wabunge wote tisa wa kaunti hiyo kugawa hela za elimu za basari kimaarifa ili watoto wanaotoka kutoka familia maskini wafaidike.
Ongwae aliomba wale ambao wamefaidika na pesa hizo za basari wasikabidhiwe pesa zile za ustawi maeneo bunge CDF ili kila mwanaafunzi afaidike.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Kisii katika hafla ya kutia sahihi kandarasi ya utendakazi baina ya waziri wa serikali ya kaunti, Ongwae alisema pesa hizo za ziada lazima ziwafaidi watoto ili kuendeleza masomo yao, na akawaomba wabunge kuwa makini wanapozigawa ili wale wanafaidika kutoka zile za kaunti wasifaidike pia na zile za eneo bunge.
Gavana Ongwae aliahidi kuongeza pesa hizo za basari kutoka Shilingi milioni tatu had milioni tano katika kila eneo la uwakilishi wadi katika kaunti hiyo.
Ongwae aidha alisema kuwa atajitahidi kwa kila awezalo ili kuona kila mtoto kutoka kaunti ya Kisii anapata elimu, na kila shule inafaidi kutokana na hela hizo ambazo zimewekwa mahususi kwa masuala ya ufadhili wa wanafunzi kielimu.
“Mimi kama gavana wa kaunti hii naunga mkono elimu na niko nyuma yenu, lakini sharti mfuate njia ambayo inakubalika wakati mnagawa pesa za basari ,” alisema Ongwae.