Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho amehimizwa kuidhinisha uchunguzi katika Wizara ya Mazingira na Raslimali za maji katika kaunti hiyo ili kuukabili ufisadi katika wizara hiyo.
Mwakilishi wa Wadi ya Changamwe katika bunge la Kaunti ya Mombasa Jimmy Odar amesema kwamba ufisadi unachangiwa na matajiri kwa kuunganishiwa maji kwa njia ya mkato, ambapo kumechangia huduma duni za usambazaji maji.
Akizungumza katika kongamano na wadau mbalimbali wa uwekezaji katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumapili, odari alisema kwamba wizara hiyo imeshindwa kusimamia shughuli za maji katika kaunti hiyo.
Odar ameshikilia kwamba ni lazima kampuni ya usambazaji maji Kaunti ya Mombasa kuwajibika na kuhakikisha kwamba kila mkazi wa kaunti hiyo anapata maji safi nyumbani kwake.
“Kukithiri kwa ufisadi katika afisi za serikali za kaunti kumechangia hata usambazaji maji kwa wakazi kuwa duni kwa sababu wengi wao hujihusisha na matajiri na kuwasambazia maji kwa njia ya mkato huku wakazi wakizidi kuteseka,” alisema Odari.
Katika siku za hivi karibuni, wakazi wa Kaunti hiyo ya Mombasa wamekumbwa na uhaba mkubwa wa maji, huku wengi wakitegemea maji ya visima.