Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia ufadhili kutoka kwa taifa la Uholanzi siku ya Alhamisi ilizindua mradi wa maji na vyoo vya kisasa kwa shule za kaunti hiyo.

Uzinduzi huo uliofanyika katika shule ya msingi ya Mrima huko Likoni ulilenga takriban shule 30 za kaunti hiyo, ambapo wanafunzi watapewa mafunzo maalum jinsi ya kudumisha usafi katika shule zao.

Serikali ya kaunti hiyo inasema kuwa imepokea ufadhili wa kiasi cha shilingi milioni 600 kutoka Uholanzi, ambapo milioni 300 zitatumika katika awamu ya kwanza ya mradi huo.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema kuwa serikali yake itajitahidi kuweka usafi mashuleni ili kuwakinga watoto na jamii kwa ujumla kutokana na maradhi ya kipindupindu.

“Sote tunajua kwamba akina mama pamoja na watoto ndio watu wa kwanza wanaoathirika kunapozuka maradhi, hivyo basi tumeamua kupatia shule zetu nafasi ya kwanza katika harakati hii ya kudumisha usafi,” alisema Joho.

Gavana Joho alisema licha ya kwamba wametenga shule 30 zitakazofaidi kutokana na mradi huo, wameamua kuipa wilaya ya Likoni kipa umbele na kutenga fursa ya shule tisa eneo hilo kwani limeathirika zaidi.

Kwa upande wake naye balozi wa Uholanzi humu nchini Frans Makken aliyehudhuria hafla hiyo alisema kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana na kaunti ya Mombasa kufanikisha maendeleo mbalimbali.

“Tunapojitahidi kufanikisha malengo ya mwaka 2030 humu nchini, lazima pia tuhakikishe kwamba kila mtoto anapata maji safi na kukaa katika mazingira bora ili kuwakinga na changamoto ya maradhi,” aliongezea balozi huyo.

Uzinduzi huo umekuja siku kadhaa baada ya kuripotiwa kuzuka kwa maradhi ya Kipindupindu katika kaunti hiyo ya Mombasa, huku Likoni ikionekana kuathiriwa zaidi ambapo watu wa familia moja walilazwa hospitalini.