Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu ametaka wadau katika sekta ya fedha na uwekezaji nchini kuingilia kati na kushawishi benki kote nchini kupunguza riba zao.
Akihutubu ofisini mwake mjini Eldoret, Gavana Jackson Mandago alisema riba ya juu ambayo benki hutoza imewafanya Wakenya wengi haswa wale wa matabaka ya chini kuogopa kuchukua mikopo ya kujiendeleza.
“Kaunti kama hii yangu inategemea ukulima kujiendeleza. Kinaya ni kwamba wakulima wengi hawachukui mikopo kutoka benki kutokana na riba ya juu. Hali hii imewanyima wakulima wengi nafasi ya kupanua uzalishaji wa chakula,” alisema Mandago.
Mandago alitaka kampuni za bima kama vile AMACO kuanzisha benki ambazo zitalipisha riba kidogo ili kusaidia wakulima.
“Sisi kama kaunti tunafikiria na kujadili uwezekano wa kuanzisha benki ya kaunti ambayo itajali maslahi ya wananchi mashinani, kwa kutoa huduma afueni za mikopo kwa wananchi,” alisema Mandago.
Gavana Mandago aliwataka Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuingilia kati na kunusuru wananchi ambao alidai wanapunjwa na benki.
Wakati huo huo Gavana Mandago aliitaka bajeti ya kitaifa kuongezea wizara ya kilimo fedha zaidi ili kuafikia mkataba wa Maputo ambao unataka mataifa wanachama kutengea sekta ya kilimo aslimia 10 ya bajeti yote ya kitaifa katika mwaka ujao wa 2016.
Hata hivyo, gavana huyo aliahidi kuwa utawala wake utatengea sekta ya kilimo fedha zaidi ili waweze kujiimudu kimaisha.