Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema kuwa serikali yake imejitolea kuwasaidia kina mama wa kaunti hiyo ili kujiimarisha kimaisha. 

Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa za kuwasaidia kina mama wa maendeleo ya wanawake kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Nyamira, Nyagarama aliwapa changamoto kina mama kutia bidii maishani ili kujistawisha kiuchumi kwa kuwa kina mama wengine katika kaunti zingine wanaendelea kuimarika hata zaidi kwa kujitolea kwao kujiendeleza. 

"Kina mama wengine kutoka kaunti zingine wamejiimarisha sana kiuchumi inafaa nanyi mtie bidii kuhakikisha kuwa mnaimarisha maisha yenu kiuchumi," alisema Nyagarama. 

Nyagarama ameongeza kusema kuwa anatarajia kina mama wa kaunti hiyo watabuni vyama vya ushirika vitakavyowasaidia kuchukua mikopo, kununua mabasi ya kina mama na vile vile shule za kina mama kujengwa. 

"Natumai kuwa mtatia bidii ili kujistawisha kimaisha, na ninataka kuona vyama vya ushirika vya kina mama vikibuniwa ili kina mama wawezeshwe kuomba mikopo na hata pia kununua mabasi ya chanzo cha maendeleo ya wanawake," alisema Nyagarama. 

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na mwakilishi wa kina mama kwenye kaunti ya Nyamira Alice Chae, mwakilishi wa kina mama kutoka Nandi Zipporah Kering, wa Bomet Cesilia Ngetich na mwakilishi wa kina mama kutoka kaunti ya Kisii ilifanikisha kuchangisha zaidi ya shillingi elfu mia 800,000.