Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa Chama cha maslahi ya wahudumu wa matatu kanda ya Pwani Sammy Gitau amependekeza kufunguliwa mashkta kwa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma yasiyo na vidhibiti mwendo badala ya kulichukulia kosa kuwa la trafiki na kuzidisha ufisadi barabarani.

Gitau alisema kuwa kuendelea kushuhudiwa kwa maafisa wa trafiki kuitisha hongo na kuyaachilia magari ya uchukuzi yasiyo na vidhibiti mwendo huenda ikaongeza idadi ya ajali barabarani.

Akiongea na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumanne, Gitau alisema kuwa iwapo hakutakuwa na sheria mwafaka, basi ufisadi baina ya maafisa wa trafiki na wahudumu wa magari ya umma utakita mizizi.

"Tunaitaka wizara ya uchukuzi na miundo msingi nchini kurejesha sheria za michuki ili kuzuia ongezeko la ajali za barabarani kwani ajili nyingi zinazotokea ni kutokana na magari ya uchukuzi wa umma kukosa vidhibiti mwendo," alisema Gitau.

Alipendekeza sheria zilizoidhinishwa na aliyekuwa waziri wa uchukuzi na miundo msingi marehemu John Michuki kurudishwa kwani kulingana na Gitau, ndizo sheria madhubuti.

Kauli ya mwenyekiti huyo imejiri huku msako mkali dhidi ya magari ya uchukuzi wa umma yaliyo na michoro ukizidi kuendelea katika Kaunti ya Mombasa ili kuhakikisha kuwa usalama wa barabarani unaimarishwa.