Balozi wa Marekani nchini Robert Godec amesema kuwa serikali yake ina imani na taifa la Kenya na kuwa itazidi kufanya kazi na taifa hili ili kufanikisha shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne alipotembelea makavazi ya Fort Jesus, Godec, ambaye aliandamana na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Alli Hassan Joho na mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff, alisema kuwa serikali ya Marekani inaunga Kenya mkono katika vita dhidi ya ugaidi.
‘’Marekani inatambua hatua ambayo Kenya imepiga katika vita dhidi ya ugaidi na uhalifu, tutashirikiana ili tuhakikishe kuwa vita hivi vinamalizwa kabisa,’’ alisema Godec.
Siku ya Jumamosi, serikali ya Marekani ikishirikiana na serikali ya Kenya ilitoa pesa zitakazofadhili upanuzi wa baadhi ya barabara mjini Mombasa kwa lengo la kuboresha uchukuzi.
Godec aliongeza kuwa Marekani itazidi kufadhili miradi mbali mbali ya maendeleo nchini ili kuchangia kubuni nafasi za ajira kwa Wakenya.
Kwa upande wake, Gavana Joho aliipongeza Marekani kwa kuondoa kikwazo cha kusafiri kilichowawekea wananchi wake huku akitaja hatua hiyo kama inayosaidia kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Aidha, mbunge wa Mvita Abdulswamad aliwahimiza wawekezaji kuwekeza mjini Mombasa na kusema kuwa hali ya usalama mjini humo kwa sasa umeimarishwa.