Sasa itakuwa ni afueni kwa wakaazi wa mitaa mbalimbali viungani mwa mjini Nakuru ambao wamekuwa wakisumbuliwa na mdudu mvyonza damu kunguni.
Wanasayansi wameorodhesha vinasaba (strands) vya DNA vya kunguni ili kusaidia kumuangamiza mdudu huyo, ambaye amekuwa akijenga kinga dhidi ya dawa za wadudu.
Matokeo yanaonyesha mdudu huyo anavyoweza kuishi kwa kutengeneza viumbe vinavyokabiliana na sumu ya dawa hizo.
Mdudu huyo pia ameanza kumea ngozi nzito ambayo huwasaidia kujilinda dhidi ya shambulio la kemikali. Hata hivyo kuna awamu ya maisha yake ambayo huenda ikawa rahisi kumuua.
Huyo ni kunguni mdogo ambaye hajawahi kuonja tone la damu ya binaadamu.
Haya ni kulingana na makundi mawili ya wanasayansi walio na kambi zao kuu katika jengo la makumbusho la Marekani, Chuo kikuu cha Cincinati pamoja na Taasisi ya Baylor mjini Texas.
Itakumbukwa kuwa mitaa ya Kaptembwa, Kwa Rhonda na Bondeni siku za hivi karibuni imekuwa ikikumbwa na janga la kunguni ambao hadi kufikia sasa bado wanashuhudiwa maeneo hayo.
Ikiwa wanasayansi hao watafaulu kuitengeneza dawa hiyo basi itakuwa ni afueni kwa wakaazi wa mitaa hiyo ambao wanasema wamejaribu kila njia na dawa zote kumuangamiza mdudu lakini yote yameambulia patupu.
Kunguni huishi kwa kunywa damu ,na ni hadi mdudu huyo anapoanza kula ndiposa baadhi ya vinasaba vyake vya DNA vinavyomlinda dhidi ya dawa hizo huanza kujiimarisha.