Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeeleza kutoridhishwa kwake na maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu ya Mombasa siku ya Jumatatu dhidi ya maafisa wa polisi waliohusika na mauaji ya msichana mwenye umri wa miaka 14 Kwekwe Mwandaza.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama muda mchache baada ya maamuzi hayo kutolewa, afisa mratibu wa mipango katika shirika hilo, Francis Auma Gamba, alisema kuwa hukumu ya miaka saba waliopewa Inspekta Veronicha Gitahi na Konstabo Issa Mzee sio wa haki kwa familia ya marehemu.
“Miaka saba ni kidogo sana kwa watu walioua mtu asiye na hatia. Tunataka kujua kwa nini maamuzi haya yanaegemea upande mmoja. Hii si haki hata kidogo kwa waathiriwa,” alisema Gamba.
Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu sasa anaitaka serikali kuingilia kati kesi hiyo ili kuhakikisha kuwa familia ya msichana huyo inapata haki, baada ya mahakama kulikataa ombi la afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma lililopendekeza kuwa maafisa hao waifidie familia ya marehemu.
Katika maamuzi yake siku ya Jumatatu, Jaji wa mahakama kuu ya Mombasa, Martin Muya, aliwahukumu kifungo cha miaka saba kila mmoja, maafisa wa polisi Veronicha Gitai na Issa Mzee baada ya wawili hao kupatikana na hatia ya kumuua Kwekwe Mwendaza mwezi Agosti 2014, katika eneo la Kinango, Kaunti ya Kwale.