Halmashauri ya Bandari nchini KPA imewahakikishia wawekezaji kutoka Bara la Afrika wanaotumia Bandari ya Mombasa usalama dhabati ndani na nje ya bandari.
Kulingana na Maneja msimamizi wa bandari Twalib Khamis, zaidi ya kamera 250 za CCTV katika eneo hilo zimewekwa huku maafisa wa usalama wakishika doria kikamilifu kutokana na kushughudiwa kwa misukosuko ya ukosefu wa usalama nchini.
Akiongea katika kongamano la kibiashara lililowajumuisha wanahabari kutoka idhaa mbalimbali barani Afrika katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumatano, Bw Khamis alisema shughuli za uchukuzi na upokeaji na usafirishaji wa mizigo imeimarisha kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na hapo awali.
Alisema kwa ushirikiano na idara ya usalama nchini pamoja na vitengo mbalimbali vya usalama barani Afrika, usalama katika bandari hiyo umeimarishwa licha ya kuwepo kwa tahadhari za kiusalama nchini.
"Kama viongozi wakuu wa Bandari ya Mombasa tumejitahidi kuimarisha usalama katika bandari yetu ili kuona kwamba biashara zinazotekelezwa na wawekezaji wetu zipo salama kwa hivyo tunashirikiana na idara ya usalama nchini na vitengo mbalimbali vya usalama barani afrika," alisema Bw Khamis.
Kauli ya meneja huyo imejiri siku chache baada ya Inspekta mkuu Generali wa Polisi nchini Joseph Boinnet kutoa tahadhari ya ugaidi nchini na kuwashinikiza wananchi kutoa habari kuhusu washukiwa wa ugaidi na kutiwa nguvuni ili taifa hili kuwa salama.