Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali kupitia kwa wizara ya elimu inasema kuwa gharama ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika shule za umma nchini inafaa kusimamiwa na fedha za hazina ya CDF badala ya shule husika.

Fedha hizo za hazina ya maendeleo hutolewa katika kila eneo bunge kuendeleza miradi ya maendeleo na sasa serikali inasema kuwa shule za umma zinafaa kufaidika na fedha hizo ili kuwapunguzia wazazi mzigo wa kuendeleza shule.

Akiongea siku ya Ijumaa wakati wa kufungua shule ya upili ya Bomu wilayani Changamwe, naibu mkurugenzi wa elimu hapa nchini James Kairo amesema kuwa hatua hiyo itaboresha zaidi shule za umma ambazo mara nyingi hubaki nyuma kimasomo.

“Wizara ya elimu imekubaliana na wabunge kwamba fedha za CDF zitatumika katika maendeleo ya shule zetu na pia kugharamia masomo ya ziada.” Alisema Bwana Kairo.

Wakati huo pia Kairo amewasisitiza wabunge wote hapa nchini kutumia vyema fedha hizo akitaja hatua hiyo kuwa ya maana katika kuboresha elimu nchini.

Serikali pia imewaonya waalimu wenye tabia ya kuongeza kiwango cha karo na mahitaji mengine yasiyokuwa muhimu kwani hali hiyo imewakandamiza wazazi kiuchumi.

“Acheni kuwaongezea wazazi mzigo kwa kuwaitisha pesa kila mara, hiyo ni hatia isiyoweza kukubalika na serikali inachunguza mambo hayo.” Aliongeza Kairo.

Naibu mkurugenzi huyo alikuwa akiongea wakati wa kufungua shule ya upili ya Bomu iliyojengwa kwa ufadhili wa hazina ya maendeleo ya CDF eneo la Changamwe ambapo pia mbunge wa eneo hilo Omar Mwinyi alihudhuria.