Hazina ya ufadhili wa masomo katika eneo bunge la Nakuru magaribi imetenga shilingi milioni 12 za kuwasaidia watoto werevu, maskini na wasiyo na uwezo wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi huyu sikuya Ijumaa, mbunge wa eneo hilo Samuel Arama alisema kuwa hakuna mwanafunzi aliyepita kutoka eneo bunge hilo atakaye kosa kujiunga na shule ya upili mwaka huu kwa kukosa ufadhili.
Mbunge huyo aliongeza kuwa pesa hizo zimeongezeka kwa shilingi milioni mbili mwaka huu, akiongeza kuwa asilimia kubwa ya shule za msingi katika eneo hilo ambazo hakuzitaja zilifanya vyema katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwaka uliyopita.
Halkadhalika, alibaini kuwa shughuli ya uteuzi wa wanafunzi wanaohitaji basari hizo zitakuwa wazi na watoto waliyopita na wenye mahitahji ndiyo watakaopewa kipau mbele.
Arama amesisitiza kuwa ni kinyume cha sheria kwa mwanafunzi yeyote kukosa kupata elimu, huku serikali ikijibidiisha kuona kuwa masomo katika taifa hili yanapatikana kwa urahisi.
Vilevile ameunga mkono hatua ya serikali ya kuwafadhili wanafunzi katika shule za upili kimasomo, kwa kuwalipia karo katika shule za upili.
Hata hivyo, Arama ametoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao waliyopita wafike katika afisi za eneo bunge hilo ili waweze kuchukua fomu hizo za ufadhili.