Serikali ya kaunti ya Lamu imebaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi katika kaunti hiyo wamesalia majumbani mwao kufuatia tishio la kiusalama.
Gavana wa Kaunti ya Lamu Issa Timamy amesema kuwa wanafunzi wa shule za msingi za maeneo ya Wadi ya Basuba na Lamu Mashariki, bado hawajafungua shule hadi sasa kufutia tishio la mashambulizi.
Timamy alisema kuwa itawalazimu wanafunzi hao kujiunga na shule za msingi za maeneo ya Lamu Kazkazini ili kuendelea na masomo yao katika shule za mabweni hasa Shule ya msingi ya Mokowe.
“Tunaiomba serikali kuweka usalama zaidi katika maeneo ya Lamu mashariki ili kuwawezesha wanafunzi kurejea shuleni licha ya kuwa tumeendaa mikakati mwafaka ya kuwasaidia wanafunzi hao kusoma,” alisema Timamy katika mkutano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, baada ya kukutana na viongozi wa kaunti.
Gavana huyo alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo itafanikisha majukumu ya wanafunzi hao, kwani zaidi ya vitanda na godoro 150 zimetolewa.
Alisema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hao wanatoka katika jamii ya Boni.
Shule ambazo kwa sasa hazijafunguliwa ni pamoja na shule ya msingi ya Milimani, Mararani, Basuba, Mangai na Kiangwe.