Idadi ya watu wanaofariki kwenye ajali za barabarani eneo la Naivasha imeendelea kuongezeka, baada ya watu watatu akiwemo mtoto wa miaka mitano kufariki mjini humo katika visa vya hivi punde.
Watu hao ambao walifariki katika visa vitatu tofauti walipokuwa wakivuka barabara wakati mikasa hiyo ilipowapata.
Mwanamume mmoja alikuwa akivuka barabara eneo la Nyondia kabla ya kugongwa na matatu iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi, huku mtoto akigongwa na gari eneo la Kayole.
Kisa cha tatu kilitokea pale mwanamme mwingine alipogonwa kwenye barabara ya Nairobi kueleke Nakuru siku ya Jumapili.
Kiongozi mmoja wa eneo hilo, James Kabono, ametaka suluhu la kudumu kutafutwa na serikali ili kuweza kupunguza maafa yanayotokana na ajali eneo hilo.
“Tunataka serikali ifanye kila jitihada kuhakikisha ajali zinazofanyika katika eneo hili zimeisha kabisa,” alisema Kabono.
OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amedhibitisha matukio hayo huku akisema madereva waliosababisha ajali hizo wanasakwa.
Munyoki vile vile amewataka madereva kuwa waangalifu hususan msimu huu wa likizo ambapo wakenya husafiri wakielekea maeneo tofauti nchini.