Idara ya watoto wilayani Molo imetakiwa kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya wafanyibiashara wanaowajiri watoto kama wafanyikazi wao, ikiripotiwa kwamba kumekuwa na ongezeko la idadi ya watoto ambao wanaacha shule mjini humo na kugeukia ajira.
Wakazi mjini Molo wamesema idara ya watoto imefeli kudhibiti idadi kubwa ya watoto wanaozurura ovyo mjini humo na baadaye kujiunga na vikundi vya uhalifu pamoja na uraibu na dawa za kulevya.
Kiongozi mmoja wa kidini mjini humo Jackson Anguza, amesema idadi ya vijana wa mitaani imeongezeka jambo ambalo linachangiwa na wafanyibiashara ambao huwapa kazi na chakula badala ya kuwahamasisha kwenda shule.
“Ofisi ya watoto pamoja na polisi wachukulie hatua wanabiashara wanaowapa watoto wasio na vitambulisho kazi ili wawape chakula na pesa kidogo. Pia kuna wazazi ambao wanatuma watoto katika mitaa ya mji waombe pesa ili wapeleke nyumbani jioni, wachukuliwe hatua,” alisema bwana Anguza
Bw Anguza amesema kwa miaka ya hivi karibuni idadi ya watoto wanaoacha shule na kugeukia vibarua wakiwa na umri mdogo imeongezeka huku akiitaka serikali kuwarejesha makwao, na warudishwe shuleni.
Amesema baadhi ya wazazi wametelekeza majukumu yao na kuacha watoto wakijitawala ambapo wao hujitoza mjini na kuchapa vibarua huku wakiombaomba pesa kutoka kwa wapita njia.
“Hawa ndio watu ambao wakizoea maisha ya mijini na pesa za haraka, watageuka na kuwa wezi au wahalifu sugu,” aliongeza.