Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mamlaka ya forodha na utoaji ushuru nchini kwenye bandari kuu ya Mombasa imeweka mikakati ya saa ishirini na nne ya kuangalia na kufuatilia shehena zinazopakuliwa na kusafirishwa katika nchi jirani ili kuona kwamba visa vya kurubuniwa kwa mali ya wateja vinakomeshwa.

Haya ni kwa mujibu wa kamishna wa forodha na ulipaji ushuru kwenye bandari ya Mombasa Julius Musyoki, ambaye amesema kuwa idara hiyo inajitolea ipasavyo ili kuzuia ukora wa matapeli ambao wanaendelea kuchukua njia za mkato na kupakua mali ya watu kutoka kwenye makasha hasa yanayoelekea nchi jirani ya Uganda.

Kamishna huyo alionya wale ambao wanaendeleza mtindo huo kuwa watanaswa na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria ya nchi na kuhakikishia wote wanaotumia bandari hiyo kuwa bidhaa zao ziko salama na idara yake inafanya bidii kuona kuwa kila mmoja anapokea bidhaa zake zikiwa salama.

Alidokeza kuwa idara yake imeweka utaratibu wa kufuatilizia mali na kulindwa kwa saa ishirini na nne ili kuwazuia baadhi ya watu ambao wamekuwa wakihudumu kama mawakala na baadaye hujihusisha na hulka ya kufungua makasha ya wateja na kutoa mali yaliyomo na kuuza.

Anasema haya siku chache tu baada ya usimamizi huo kunasa magari matatu aina ya Range Rover ambayo yanaaminika kuwa ya makasha ambayo yalikuwa yasafirishwe kuelekea nchi ni Uganda.