Mwendo wa kobe katika kutatua kesi zinazohusu watoto zimepelekea baadhi yao kusalia katika vituo vya kurekebisha mienedo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Jambo hilo limefichuliwa na Lorna Sang, meneja wa kituo cha urekebishaji tabia katika kaunti ya Nakuru kilicho katika eneo la Bondeni, viungani mwa mji wa Nakuru.
Alisema kuwa kulingana na sheria, mtoto anayepelekwa kwenye kituo hicho anafaa kukaa kwa muda wa miezi mitatu tu.
Akiongea na mwandishi huyu ijumaa katika mahojiano ya kipekee, ametoa mfano wa mtoto mmoja ambaye amekaa kwenye kituo hicho kwa muda wa miaka mitatu sasa baada ya kesi yake kuahirishwa mara kadhaa.
Akiangazia kuhusiana na kituo hicho, Sang alieeleza kuwa wajibu wao mkuu ni kuwasaidia watoto hao kurekebisha mienedo kwa kuwapa mawaidha, akisema kuwa kuna wafanyikazi kumi na watano katika kituo hicho huku kila mfanyikazi akiwa na jukumu lake la kuwahudumia watoto hao.
Kando na kuwapa mawaidha, wafanyikazi wengine huwapa mafunza tofauti yanayoweza kuwasaidia maishani pamoja na kuwapatanisha watoto waliotoroka nyumani na familia zao.
Wakati huo huo, ametaoa wito kwa idara ya mahakama kujibidiisha na kuhakikisha kuwa kesi zinazohusu watoto hao zinatatuliwa haraka iwezekanavyo.