Idara ya trafiki mjini Nakuru imewapongeza madereva na makanga wa magari ya umma kwa kudumisha nidhamu ya hali ya juu wakati wa msimu huu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya.
Afisa mkuu wa trafiki eneo la bonde la ufa Mary Omari amesema kuwa madereva na makanga wameonyesha nidhamu ya hali ya juu ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akizungumza Jumatatu mjini Nakuru Omari alisema kuwa visa vya utovu wa nidhamu barabarani na hata ajali vimepungua kwa kiasi kikubwa.
Omari alisema kuwa hilo limetokana na hatua ya wengi wa madereva kuzingatia sheria za trafiki na juhudi za maafisa wa trafiki.
"Tukilinganisha na misimu iliyopita, msimu huu madereva wetu wamekuwa na nidhamu sana na hatujarekodi visa vingi vya ajali ama utovu wa maadili," alisema Omari.
"Kama idara tunawapongeza madereva wote na watumizi wengine wa barabara ambao wamefanya barabara zetu zikawa salama wakati huu wa sherehe," aliongeza Omari.
Afisa huyo aliwataka madereva kudumisha mtindo huo wa kuzingatia sheria za trafiki kila wakati ili kupunguza idadi ya ajali barabarani.
"Kama madereva wanaweza kuwa waangalifu jinsi walivyofanya msimu huu basi tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa maafa katika barabara zetu," alisema Omari.