Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC wameanzisha vikao vya hamasa kuhusu umuhimu wa usajili wa wapiga kura katika kanda ya Pwani kaskazini ili kufanikisha zoezi hilo.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Mombasa, mshirikishi mkuu wa tume hiyo kanda ya Pwani kaskazini Amina Sudi amesema kuwa zoezi hilo la hamasisho kwa jamii ya Wapwani litasaidia pakubwa kuongeza idadi ya wapiga kura kwani kwa sasa waliojitokeza kwa zoezi hilo ni wachache mno ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Amina alisema kuwa tayari maafisa wa tume hiyo wamezuru mashinani kufanya vikao vya hamasa kwa jamii kwani wengi wao wanapotoshwa na baadhi ya makundi fulani yanayolenga kuvuruga zoezi hilo muhimu nchini.
“Tumeonelea tuzuru mashinani kuwahamasisha wakaazi kufahamu umuhimu wa zoezi hili kwani wengi wa wakaazi wa eneo hili bado wangali nyuma katika kufahamu umuhimu wa zoezi hili. Wanashauriwa vibaya na baadhi ya watu fulani wenye nia ya kuvuruga zoezi hili lakini tunaimani kuwa tutafikia kiwango tulichopanga,” alisema Sudi.
Wakati huo huo, amewataka viongozi wa kisiasa kutoliingiza siasa zoezi hilo na badala yake kuwaunga mkono maafisa wa tume hiyo pamoja na kuwashuari wakaazi wa eneo la pwani kujitokeza kusajiliwa kuwa wapiga kura.
Tunawaomba viongozi wa kisiasa kutusaidia katika kuwahamasisha wakaazi kufahamu umihumu wa zoezi hili na kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kama wapiga kura badala ya wao kuliingiza siasa zoezi hili,” aliongeza Sudi.
Zoezi hilo limeingia wiki yake ya tatu, huku idadi ya wakazi wanaojitokeza kusajiliwa kama wapiga kura ikionekana kuwa ndogo.