Tume huru ya mipaka na uchaguzi nchini IEBC imemkashifu vikali mwanasiasa ambaye pia ni mfanyibiashara mjini Mombasa Suleiman Shahbal kwa kutoa matamshi yanayoweza kuleta mgawanyiko wa kikabila na kuzua chuki miongoni mwa Wakenya.
Akizungumza mjini Nairobi siku ya Jumatano, mwenyekiti wa IEBC Issack Hassan, amewaonya wanasiasa wanaolenga kuvuruga amani kwa kutoa matamshi ya uchochezi kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuwafungia nje katika uchaguzi wa 2017.
Hassan ameyataja matamshi ya Shahbal kuwa ''muungano wa Jubilee utashinda uchaguzi wa 2017 kwa ulazima hata kama ni kuiba'' kuwa hatari kwa usalama wa nchi na yanaweza kulitumbukiza taifa kwenye lindi la vita vya wenyewe kwa wenyewe.
''Kama IEBC kazi yetu ni kuhakikisha kuwa tunausimamia uchaguzi uhuru na wa haki kwa kila Mkenya,'' alisema Hassan.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa matamshi ya Shahbal yamekiuka katiba na kuvunja kipengele 62, 63 na 64 cha sheria na hivyo lazimu akabiliwe kwa mujibu wa sheria.
Kauli ya Hassan yanajiri saa chache tu baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma Kiriako Tobiko kuiagiza tume ya IEBC na idara ya upelelezi nchini CID kuanzisha uchunguzi kuyahusu matamshi ya mwanasiasa huyo.
Suleiman Shahbal ambaye alijiunga na Jubilee hivi majuzi baada ya kugura chama cha Wiper, aliyatoa matamshi hayo katika mkutano wa kisiasa uliohudhuriwa na Naibu Rais William Ruto mjini Malindi siku ya Jumamosi wikendi iliyopita.