Kufuatia kuwepo kwa tetesi kwamba baadhi ya wanasiasa katika eneo bunge la Borabu wamekuwa wakijuhusisha na usafirishaji wa wapiga kura kutoka maeneo ya nje, mwanasiasa mmoja amejitokeza kuitaka tume ya IEBC kuhairisha usajili wa wapiga kura katika katika eneo hilo.
Akihutubia wakazi wa Magura siku ya Jumatano, Dkt Nyandoro Kambi aliitaka tume hiyo kusitisha uandikishaji wa wapiga kura mara moja.
Kambi alitishia kuwataja wanasasia wanao jihusisha na usafirishaji wa watu wasio wakaazi wa eneo hilo iwapo tume ya IEBC itadinda kusitisha shughuli hiyo ya usajili.
"Sharti tume ya IEBC isimamishe uandikishaji wa wapiga kura mara moja hadi pale watakapo tueleza sababu ya wanasiasa wengine kusafirisha wakaazi wa maeneo mengine ya bunge kujisajili huku Borabu kama wapiga kura. Eneo bunge hili lina wakaazi wanaostahili kufanya maamuzi wakati wa uchaguzi na niko tayari kuwataja wanasiasa wanao jihusisha na usafirishaji huo," alisema Kambi.
Kambi ambaye pia ana nia ya kuwania ubunge katika eneo hilo la Borabu, alidai kuwa baadhi ya wapiga kura kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba na Mugirango Magharibi wamekuwa wakisafirishwa na wanasiasa fulani ili kujisajili katika eneo hilo, baada yao kuhaidiwa kulipwa.
"Kwa kweli watu ambao wamekuwa wakisafirishwa kujisajili kama wapiga kura katika eneo hili sio wakaazi wa Borabu. Ni watu tu wanaolipwa na baadhi ya wanasiasa ili kujisajili kama wapiga kura huku na kamwe hilo halitakubalika," alisema Kambi.
Kambi aidha alidai kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kuitumia vibaya tume ya IEBC kwa manufaa yao, suala alilosema limemlazimu kumwandikia barua mwenyekiti wa kitaifa wa tume hiyo Isaac Hassan, kulalamikia hali.
Aliipa changamoto tume hiyo tawi la Nyamira kuweka bayana orodha ya wapiga kura wa hivi maajuzi ili kuthibitisha madai yake.
"Uchaguzi huwa tu huru wakati wenyeji wanapopewa nafasi ya kufanya maamuzi bila ya kuwahusisha watu wanaotoka maeneo bunge ya nje. Nimemwandikia barua mwenyekiti wa IEBC Isaac Hassan ili kulalamikia usajili huu," alisema Kambi.