Tume huru ya Uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC imesema kuwa imejiandaa vyema katika uchaguzi mdogo wa Malindi huku wakisema kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Mshirikishi mkuu wa tume hiyo kanda ya pwani kazkazini Amina Soud amesema kuwa zoezi hilo la uchaguzi limeandawa kikamilifu na maafisa wa Tume hiyo wamejiandaa kufanikisha shughuli hiyo bila pingamzi.
Akiongea na wanahabari katika afisi za tume hiyo mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Amina amesema maafisa wa tume hiyo watakaosimamia shughuli hiyo wamepata mafunzo bora zaidi jinsi ya kutekeleza shughuli hiyo na akahimiza kuwa shughuli hiyo itafanyika vyema.
Afisa huyo wa IEBC amewahimiza wakaazi wa eneo bunge hilo kuhakikisha kuwa wanajitokeza kwa upigaji kura huo ili kuona kuwa shughuli hiyo inafanyika vyema na kukamilika mapema huku akisema kuwa maafisa wa tume hiyo watafungua vituo hivyo asubuhi ya saa mbili.
“Tunawahakikishia wakaazi wa eneo bunge la Malindi kuwa uchaguzi huo mdogo utakuwa huru na haki kwa wakaazi wa Malindi na tunawaomba wakaazi wajitokeza mapema ndio shughuli ya kuhesabu kura ikamilike mapema,” alisema Amina.
Wakati uo huo amewahakikishia wakaazi wa eneo hilo usalama dhabiti akisema kuwa idara ya usalama ikishirikiana na maafisa wa tume hiyo wamejiandaa vyema kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inafanyika vyema.
“Tunawahakikishia wakaazi wa eneo la Malindi kuwepo na usalama dhabiti wakati wa shughuli hiyo ya upigaji kura kwani maafisa zaidi wa usalama kwa sasa wameanza kushika doria eneo hilo ili kufanikisha zoezi hilo kwa njia ya amani na uchaguzi huru,” aliongoza Amina.