Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa maeneo ya Lamu na Malindi watashiriki kwenye usajili wa wapiga kura hivi karibuni, baada ya kukamilika kwa shughuli ya usajili wa wapiga kura unaoendelea sasa nchini.

Kulingana na mshirikishi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka eneo la Pwani Kaskazini, Amina Soud, aidha wakaazi wa maeneo hayo watatengewa muda wa mwezi mmoja ili nao wasajiliwe kama ilivyofanyika katika maeneo mengine nchini.

Akiongea na wanahabari siku ya Ijumaa mjini Mombasa, Amina alisema kuwa eneo bunge hilo halikushirikishwa katika shughuli ya usajili unaoendelea kutokana na harakati za maandalizi ya uchaguzi mdogo, ambao ulifanyika siku ya Jumatatu.

Kaunti ya Lamu ilikosa kushirikishwa kutokana na kesi ambayo iliwasilishwa mahakamani na mwanasiasa Fahim Twaha, aliyepinga uteuzi wa Gavana wa kaunti ya Lamu Issa Timamy, japo kesi hiyo ilisikizwa na kuamuliwa.

“Tutafanya usajili wa wapiga kura Malindi na Lamu kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na shughuli za maandalizi ya uchaguzi Malindi na kesi ya Timamy kuhusu uchaguzi wake kwa sababu tunataka kila Mkenya kusajiliwa na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu ujao," alisema Amina.

Hata hivyo Amina Soud amewahimiza wakaazi wa maeneo ambako usajili huo unaendelea wajitokeze ili wasajiliwe kabla ya shughuli hiyo kukamilika mnamo tarehe 15 mwezi huu.