Tume huru ya uchaguzi na mipaka eneo la Central Rift imewataka machifu na wazee wa mpango wa Nyumba Kumi kujtokeza na kuwahamasisha raia kujisajili kama wapiga kura.
Mshirikishi wa IEBC wa tawi hilo David Towett amesema kuwa machifu na wazee wana jukumu kubwa la kutekeleza katika uhamasisho wa wapiga kura.
Akizungumza Jumamosi mjini Nakuru, Towett aliwataka wazee na machifu kutumia ushawishi walio nao kuwarai watu kujisajili kwa wingi kama wapiga kura.
Towett aliongeza kuwa iwapo machifu na wazee watatembea katika kila kijiji wakiwahamasisha watu, basi idadi ya watu wanaojisajili itaongezeka maradufu.
"Ninatoa wito kwa wazee wa Nyumba Kumi na machifu wajitokeze na kutusaidia katika kuwahamasisha watu katika vijiji ili wajitokeze na kujisajili kwa wingi kama wapiga kura," alisema Towett.
"Machifu na wazee wataa wako karibu na raia na wanaweza kuwashawishi waende wakajisajili kwa wingi," aliongeza.