Share news tips with us here at Hivisasa

Mshukiwa wa mauaji ya wafanyibiashara wa ngono mjini Nakuru, Jumatatu hakujibu mashtaka dhidi yake baada ya jaji Maureen Odero aliyekuwa akisikiliza kesi dhidi yake kukosa kufika mahakamani baada ya kuwa na kazi nje ya mahakama hiyo.

Ashton Wachira alishtakiwa katika mahakama ya juu ya Nakuru akidaiwa kuhusika na mauaji ya Maureen Wanjiru almaarufu kama Wahu, usiku wa Jumapili tarehe 17, Januari, 2016 katika mtaa wa Freehold mjini humo.

Alishtakiwa kutekeleza mauaji hayo katika wakati ambapo wafanyibiashara wa ngono walikuwa wakiandamana barabarani kulalamikia mauaji ya wenzao wapatao wanane katika muda wa mwaka mmoja uliopitta.

Takriban wiki mbili zilizopita jaji Odero aliamrisha mshukiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili, haswa baada ya mshukiwa kumtaka jaji huyo kubadilisha jina lake.

Wachira alirejeshwa katika rumande ya gereza kuu la serikali mjini Nakuru, kama ilivyoagiza mahakama.

Jaji Anthony Ndung’u aliorodhesha tarehe 8, Februari 2016, kama siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.