Wasichana wanne wanaokabiliwa na madai ya ugaidi wanamtaka jaji mkuu Dkt Willy Mutunga kuteuwa jopo la majaji watatu kusikiliza kesi yao kwa haraka.
Kupitia kwa wakili wao Hamisi Mwadzogo, wasichana hao wamewsilisha ombi la dharura katika mahakama kuu ya Mombasa na kwa jaji mkuu ili kusisitiza kuteuliwa kwa jopo hilo ili haki na usawa kupatikana kwa wateja wake.
Mwadzogo alisisitiza kuwa kufikia sasa, upande wa mashataka unajikokota katika kuendesha kesi hiyo, jambo alilolitaja kama ukandamizaji wa haki za wateja wake.
Hatua hii inajiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kutaka kuwafungulia mashtaka mapya wasichana hao baada ya mahakama kuwaachilia kwa dhamana.
Hapo jana, Jumatano, mahakama kuu ilidinda kufutilia mbali dhamana ya wasichana hao, baada ya afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma kutaka dhamana hiyo kufutiliwa mbali.
Wanne hao Ummulkheir Abdullah kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 21, Mariam Said Aboud pamoja na Khadija Abubakar wenye umri wa miaka 19 wote kutoka Malindi wanadaiwa kuwa wanafunzi walioahidiwa ufadhili wa kimasomo nchini Somalia, huku Halima Aden akikamatwa katika kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi.