Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulizuka kioja cha kipekee katika kituo cha polisi cha Naivasha baada ya mwanamme mwenye umri wa makamo kujipeleka kwenye kituo hicho akitaka azuiliwe kutokana na tuhuma za kumuua babake mzazi miaka mitatu iliyopita.

Mbele ya maafisaa wa polisi, jamaa huyo alikiri kumuua babake mwaka wa 2013 katika eneo la Kinoo Nairobi, baada ya mzazi wake huyo kuuza shamba na kuitelekeza familia. 

Kisanga hicho kilivutia wakaazi wengi waliotaka kujua kulikoni, huku wakisalia na mshtuko mkubwa.

Jamaa huyo, David Mwangi, alisema badaa ya kutekeleza unyama huo akiwa na mwenzake, mawazo chungu nzima pamoja na ndoto mbaya yamemwandama, kiasi kwamba hangeweza kuvumilia tena.

“Hapo mbeleni niliambia polisi kwamba babangu, Erick Githambo, aliuawa na majambazi, na tukamzika siku tatu baadaye huko Lang’ata,” Mwangi akaambia polisi waliomhoji.

OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amedhibitisha tukio hilo, na kusema kuwa mshukiwa huyo angali anazuiliwa ili kuweza kuhojiwa zaidi akitaja kisa hicho kama cha kipekee.

Munyoki ameongeza kuwa mshukiwa amekabidhiwa maafisa wa  kituo cha polisi cha Kabete pahali ambapo kisa hicho kiliripotiwa mara ya kwanza.